Vita hatarini kuendelea baada ya Marekani kukamata meli ya Iran


SITISHO la mapigano kati ya Marekani na Iran limekuwa hatarini baada ya Marekani kusema imekamata meli ya mizigo ya Iran iliyojaribu kuvunja vizuizi vyake, huku Tehran ikiapa kulipiza kisasi huku ikikataa kushiriki mazungumzo mapya ya amani.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amesema Washington imeonyesha kuwa haina nia ya dhati ya kuendeleza mchakato wa kidiplomasia, na kwamba Tehran haitabadilisha madai yake yaliyowekwa wazi.

Ameyabainisha hayo mapema leo huku akisisitiza kuwa Iran haiamini katika kuwekwa kwa muda maalum au masharti ya lazima inapolinda maslahi yake ya taifa.

Jeshi la Marekani limesema lilifyatua risasi dhidi ya meli ya mizigo iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Iran, iliyokuwa ikielekea bandari ya Bandar Abbas Jumapili baada ya mvutano wa saa sita, na kuharibu injini zake.

Kamandi Kuu ya Marekani ilitoa video ikionyesha wanajeshi wa majini wakishuka kwa kamba kutoka kwenye helikopta na kuingia kwenye meli hiyo.

Jeshi la Iran limesema meli hiyo ilikuwa ikitoka China, huku likiishutumu Marekani kwa “uharamia wa kijeshi.”

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali, jeshi hilo lilikuwa tayari kukabiliana na majeshi ya Marekani lakini lilizuiliwa na uwepo wa familia za wafanyakazi ndani ya meli.

Tukio hilo limeifanya Tehran kukataa mazungumzo mapya ya amani kwa sasa, huku sababu nyingine ikiwa ni kuendelea kwa vizuizi, kauli za vitisho, na mabadiliko ya misimamo ya Washington pamoja na madai yaliyopitiliza.

“Huoni mantiki kuzuia mauzo ya mafuta ya Iran huku ukitarajia usalama wa bure kwa wengine. Chaguo liko wazi: ama soko huria la mafuta kwa wote, au hatari ya gharama kubwa kwa kila mtu,” Makamu wa Rais wa Kwanza Mohammadreza Aref aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

Marekani ilikuwa na matumaini ya kuanza mazungumzo nchini Pakistan muda mfupi kabla ya sitisho la mapigano la wiki mbili kuisha, huku maandalizi makubwa ya kiusalama yakiendelea Islamabad.

Hata hivyo, Baghaei amesema Marekani “inasisitiza misimamo isiyo na mantiki na isiyowezekana.

Related Posts