Trump Vs Elon MuskTrump Vs Elon Musk

VITA ya Trump na Elon Musk si ya Kitoto, Wavurugana Hadharani

Uhusiano wa karibu kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na mfanyabiashara maarufu duniani Elon Musk sasa unaonekana kufikia ukingoni, kwasababu ya kutupiana maneno makali na tuhuma nzito katika majukwaa ya mitandao ya kijamii.

Mvutano huo uliibuka hadharani baada ya Elon Musk kukosoa vikali mswada mpya wa bajeti unaosukumwa na Trump, akiuita “wa kuchukiza,” na kuongeza kuwa ni “aibu kwa waliounga mkono muswada huo.” Trump, kwa upande wake, alijibu kwa hasira kupitia ukurasa wake wa Truth Social, akitishia kufuta mikataba ya serikali inayohusiana na kampuni za Musk kama SpaceX na Tesla.

“Njia rahisi ya kuokoa mabilioni ya fedha za umma ni kusitisha ruzuku na mikataba ya kiserikali ya Elon,” aliandika Trump. “Siku zote nilishangazwa kwamba Biden hakufanya hivyo!”

Katika kujibu, Elon Musk alimshutumu Trump kwa “kutokuwa na shukrani” na kudai bila ushahidi kwamba aliisaidia kampeni ya Trump kushinda uchaguzi wake wa awali.

“Bila mimi, Trump angepoteza uchaguzi,” aliandika Musk kwenye X (zamani Twitter).

Musk pia alitangaza kuwa kampuni yake ya anga, SpaceX, itaanza kuzima shughuli za Dragon spacecraft- chombo kinachotumiwa na NASA kuwapeleka wanaanga katika anga za juu akidai kauli za Trump zinaashiria uhasama wa kisera.

Mvutano huo umezidi kuingia katika eneo lenye utata baada ya Musk kudai kuwa Trump ametajwa katika nyaraka za serikali ambazo bado hazijatolewa hadharani, zinazohusiana na mfanyabiashara aliyekufa akiwa mahabusu, Jeffrey Epstein.

Kauli hiyo imesababisha White House kutoa tamko rasmi kupitia Katibu wa Habari Karoline Leavitt, aliyesema: “Hiki ni kipindi cha bahati mbaya kwa Elon, ambaye hajafurahishwa na Mswada wa One Big Beautiful kwa sababu haujumuishi sera alizotaka.”

Kwa miaka mingi, kampuni za Elon Musk zimenufaika na mikataba ya kiserikali inayofikia takriban dola bilioni 38, ikiwemo ruzuku, mikopo, kandarasi za utafiti na motisha za kikodi, kulingana na Washington Post.

Mwezi Mei, Trump alimkabidhi Musk “funguo za dhahabu” kama ishara ya heshima kwa mchango wake katika Wizara ya Ufanisi wa Serikali — nafasi aliyoitumikia kwa siku 129 kabla ya kujiuzulu ghafla wiki iliyopita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *