
Vigogo wa soka nchini Tanzania, Simba SC na Yanga, wamefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Kombe la Muungano 2026 linaloendelea kufanyika visiwani Zanzibar.
Miamba hiyo miwili ya soka la Tanzania wanakutana katika mchezo wa fainali utakaopigwa tarehe 29 katika Uwanja wa New Amaan Complex, huku mashabiki wa soka wakisubiri kwa hamu kushuhudia pambano hilo kubwa litakaloamua bingwa wa michuano hiyo.
Simba na Yanga zimeonyesha ubora mkubwa katika michezo yao ya hatua ya robo na nusu fainali, jambo lililozifanya kufuzu hadi hatua ya mwisho ya mashindano hayo ambayo mara nyingi hutumika kama sehemu ya maandalizi kabla ya mechi muhimu za msimu.
Kinachofanya fainali hii kuwa ya kipekee zaidi ni kwamba haitakuwa mara ya mwisho kwa watani hao wa jadi kukutana katika kipindi hiki kifupi. Baada ya pambano la fainali ya Kombe la Muungano, timu hizo zinatarajiwa kukutana tena Mei 3 katika mchezo mkubwa wa Kariakoo Derby, ambao ni sehemu ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara NBC.
Hivyo ndani ya siku chache, mashabiki wa soka watapata burudani ya kushuhudia dabi mbili kubwa mfululizo kati ya Simba na Yanga, jambo ambalo linaongeza presha, ushindani na hamasa kubwa kwa pande zote mbili.
Swali kubwa linalobaki sasa ni nani ataibuka bingwa wa Kombe la Muungano kabla ya kuelekeza nguvu kwenye Kariakoo Derby ya ligi? Mashabiki wanasubiri kwa hamu kuona historia mpya ikiandikwa.
