
Rais wa Marekani Donald Trump ametoa kauli iliyozua mjadala mkubwa baada ya kuulizwa moja kwa moja kwa nini anaendelea kuwa mlengwa wa majaribio ya mauaji ya kisiasa.
Akizungumza na waandishi wa habari kufuatia tukio la hivi karibuni katika White House Correspondents’ Dinner, Trump amsema kuwa watu wenye ushawishi mkubwa ndio wanaolengwa zaidi na washambuliaji.
“Watu wanaofanya mambo makubwa zaidi, wenye athari kubwa zaidi duniani, ndio wanaolengwa,” alisema Trump, akitaja viongozi wa kihistoria kama Abraham Lincoln ambaye aliuawa mwaka 1865.
Kauli hiyo ilitolewa baada ya tukio la hivi karibuni ambapo mshukiwa alijaribu kushambulia hafla hiyo iliyofanyika Washington, akidaiwa kuwa na nia ya kulenga viongozi wa serikali. Tukio hilo ni moja ya mfululizo wa matukio ambayo yamehusisha vitisho au mashambulizi dhidi ya Trump tangu mwaka 2024.
Katika maelezo yake, Trump aliongeza kuwa washambuliaji hawalengi watu wasiofanya mambo makubwa, akisisitiza kuwa nafasi yake na maamuzi yake makubwa ya kisiasa yanaweza kuwa sababu ya yeye kuwa shabaha mara kwa mara.
Kauli yake imepokelewa kwa mitazamo tofauti. Wapo wanaomuunga mkono wakisema kuwa historia inaonyesha viongozi wenye ushawishi mkubwa mara nyingi hukumbana na hatari kubwa.
Matukio haya yameibua upya mjadala kuhusu usalama wa viongozi wa juu pamoja na mazingira ya kisiasa yanayozidi kuwa na mvutano mkubwa nchini Marekani.
Wakati huo huo, vyombo vya usalama vinaendelea kuchunguza tukio la hivi karibuni ili kubaini kwa kina nia na mazingira yaliyopelekea jaribio hilo la shambulio.
