
Watanzania 203 wamerejeshwa Nchini kutoka Mataifa mbalimbali baada ya kubainika kukiuka Sheria za Uhamiaji za Nchi walizokuwa wakiishi ikiwemo kuingia au kuendelea kuishi bila kufuata taratibu rasmi zilizowekwa.
Hayo yameelezwa leo Mei 25, 2026 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara hiyo ambapo amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria za Mataifa mbalimbali dhidi ya Wahamiaji wasiokuwa na vibali halali.
Katambi amesema kurejeshwa kwa Watanzania hao kumetokea katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na Mamlaka za Ndani na za Kimataifa kuhakikisha taratibu za Uhamiaji zinafuatwa ipasavyo.
Mbali na hilo, amesema Idara ya Uhamiaji imeendelea kushughulikia masuala ya uraia ambapo Wageni 64 wamepewa uraia wa Tanzania katika kipindi hicho huku Watanzania 17 wakikana uraia wao baada ya kupata uraia wa Mataifa mengine kwa mujibu wa Sheria ya Uraia, Sura ya 357 ya mwaka 2023.
