
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa onyo kwa baadhi ya Viongozi wanaodaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao wakisubiri uteuzi mpya.
Akizungumza leo Juni 26, 2026 Bungeni Jijini Dodoma, Waziri Mkuu amesema kuna baadhi ya Viongozi wanaishi kama “wapiga ngazi,” wakisubiri mabadiliko ya uteuzi badala ya kufanya kazi zao ipasavyo.
“Wote tunajua kuna kifo, hivi tungekuwa tunasubiri kifo kuna Mtu angefanya kazi? Unasubiri nini uteuzi wakati una jukumu la kufanya kazi?” amehoji Waziri Mkuu.
Ameongeza kuwa uteuzi usiwe chanzo cha Viongozi kukaa bila kufanya kazi au kusubiri maamuzi ya kisiasa, akisisitiza kuwa watendaji wote wanapaswa kuwajibika wakati wote.
“Nasisitiza suala la teuzi, hasa zile zinazofanyika kwa presha ya anayeteua zisiburiwe, tunataka Watu waendelee na kazi na wasiosikiliza maelekezo haya watajitambulisha kwamba hawatakiwi kuwepo maofisini,” amesema.
Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe kazini unaochochewa na kusubiri mabadiliko ya vyeo badala ya kutoa huduma kwa Wananchi.
