RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameunda Tume Huru ya kufanya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea nchini wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 29 Oktoba, 2025 ambapo amemteua Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mohamed Chande Othman kuwa Mwenyekiti wa Tume hiyo.
Rais Samia ameunda tume hiyo kwa mamlaka aliyonayo chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32 ambapo pia amewateua wajumbe saba wa tume hiyo akiwemo, Mhe. Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania na Balozi Ombeni Yohana Sefue Kiongozi Mstaafu; Mwanadiplomasia na Katibu Mkuu.
Taarifa ya leo Novemba 18, 2025 iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka imeeleza kuwa wajumbe wengine ni pamoja na Balozi Radhia Msuya – Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu; Balozi Lt. Gen. Paul Meela ambaye ni Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu; IGP (Mstaafu) Said Ally Mwema Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania Mstaafu; Balozi David Kapya – Mwanadiplomasia na Balozi Mstaafu; na Dkt. Stergomena Lawrence Tax ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

