ACT Wazalendo watangaza Baraza jipya la Mawaziri Kivuli

 


Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza rasmi Baraza jipya Kivuli la Mawaziri kwa kipindi kinachofuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikisema hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa Serikali na kuendeleza mapambano ya uwajibikaji nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu amesema matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2025 yameendelea kutoa uwakilishi mdogo wa upinzani Bungeni, hali inayovifanya vyama vya siasa kutumia mifumo mbadala ya kuisimamia Serikali nje ya Bunge.

Katika uteuzi huo, Isihaka Rashid Mchinjita ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu Kivuli huku Luhaga Mpina akiteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu Kivuli na Waziri wa Nishati na Madini. Nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi imetolewa kwa Idrisa Abdul Kweweta.

Chama hicho kimesema uteuzi huo umezingatia uwakilishi wa kitaifa pamoja na usawa wa kijinsia, ambapo wanawake ni 11 kati ya wasemaji 23 walioteuliwa, sawa na asilimia 47 ya wajumbe wote wa Baraza hilo.

Miongoni mwa walioteuliwa katika nafasi za usemaji wa kisekta ni Nagy Kaboyoka, Peter Madeleka pamoja na Elizabeth Sanga.

Katika tamko lake, chama hicho kimeelekeza Baraza Kivuli kuweka mkazo katika kusimamia uwajibikaji wa viongozi wa Serikali, matumizi ya fedha za umma na ulinzi wa haki za wananchi.

ACT Wazalendo pia kimeeleza kuwa kupitia uchambuzi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zaidi ya shilingi trilioni saba zimeonekana kupotea au kutumika bila maelezo ya kuridhisha, huku kikisisitiza kuwa hatua za uwajibikaji zinapaswa kuchukuliwa dhidi ya wahusika.

Aidha, chama hicho kimesema kitaendelea kuwa sauti ya wananchi ndani na nje ya vyombo rasmi vya dola kwa kuibua masuala ya msingi yanayowagusa wananchi, yakiwemo matumizi mabaya ya madaraka, migogoro ya ardhi na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Baraza hilo ni la tatu kuundwa tangu kupitishwa kwa azimio la mwaka 2022 lililoruhusu kuanzishwa kwa mfumo huo ndani ya chama.

Related Posts