Baba Levo Ataweza Kupambana na Zitto Kabwe Ubunge Kigoma Mjini?
Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 Zitto Kabwe alishindwa kiti cha Ubunge pale Kigoma Mjini, Mhe. Mgenda Shaban Kilumbe kutoka CCM ndiye aliibuka mshindi, alishida kura 27, 638, Zitto Kabwe 20,600. Zitto Kabwe bado hajakata tamaa, ametangaza nia na tayari amechukua fomu ya kugombea ubunge wa Kigoma Mjini mwaka 2025 kupitia chama cha ACT Wazalendo.
Baba Levo pia ametangaza kuwa atawania Ubunge jimbo hilo hilo la kigoma Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi, hivyo mjadala mkubwa hivi sasa kwenye mitandao ya kijamii ni Je, Baba Levo ataweza kweli kumpiku Mbobevu wa siasa Zitto Kabwe, ambaye tayari amewahi kuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kwa mihula miwili?
Mpaka sasa Zitto Kabwe hana kipengele kikubwa kwani ni lazima Wajumbe wa ACT wampitishe kuwa Mgombea kwa sababu ndiye mwenye ushawishi zaidi katika jimbo hilo, lakini upande wa Baba Levo bado moshi mweupe haujatoka kwani Mbunge wa sasa wa Kigoma Mjini, Mhe. Mgenda Shaban Kilumbe huenda akachukua fomu tena, je wajumbe watakuwa tayari kumpiga chini na wamchague Baba Levo ambaye hana uzoefu mkubwa kwenye siasa? Wataamini vipi kuwa Baba Levo atatetea jimbo hilo libaki chini ya CCM, kama Mhe. Mgenda Shaban Kilumbe alivyopindua meza 2020?
Tufanye wajumbe wamempitisha Baba Levo, hatimaye akafanikiwa kuwania Ubunge wa Kigoma Mjini pamoja na Zitto Kabwe, je unahisi anaweza kushinda uchaguzi na kutangazwa kuwa Mbunge wa jimbo hilo?