Katika hali ya kuonesha uzalendo na kuthamini mchango wa viongozi, msemaji wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally, amesema timu hiyo ipo tayari kumfurahisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kushinda kombe la Afrika.
Akizungumza kabla ya mechi ya fainali inayotarajiwa kufanyika Jumapili nchini Morocco, Ally aliwapongeza wachezaji kwa juhudi zao na kuwataka kuongeza bidii ili kuandika historia kwa taifa.
“Tuko tayari kumfurahisha mama yetu Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa mchango mkubwa ambao anatupatia.
Ametoa ndege bure kutupeleka Morocco na amekuwa akitoa motisha kwa kila mechi,” alisema Ally.
Aliongeza kuwa kinachobaki sasa ni kumheshimu Rais kwa kumletea kombe hilo nchini.
“Kilichobaki ni kumheshimisha mama yetu kwa kumpa kombe la Afrika na kuwa Rais wa kwanza Tanzania kubeba kombe la Afrika. Tutapeleka kombe Ikulu.”
Ahmed Ally pia aliwataka wachezaji wa Simba kujituma kwa moyo wote, kutumia maarifa na nguvu zao zote kuhakikisha ushindi unapatikana.
“Wachezaji wetu waende wakapambane wanavyoweza, Simba tuchukue ubingwa siku ya Jumapili,” alisisitiza.
Tanzania nzima sasa inasubiri kwa hamu tukio hilo la kihistoria.