Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, imetangaza kuwa iko tayari kumsamehe Mbunge wa Kawe na Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima.

Hata hivyo, msamaha huo hautolewi bila masharti, ambapo sharti kuu ni kwamba kanisa lake linapaswa kufuata taratibu rasmi za kisheria na kukata rufaa ili kufunguliwa tena.

Tangazo hili linakuja baada ya kanisa hilo kufungiwa kufuatia mzozo uliobuka baina ya Gwajima na baadhi ya viongozi wa serikali ya chama tawala, CCM.

Gwajima, ambaye pia ni mbunge kupitia chama hicho, amekuwa akikosoa hadharani baadhi ya maamuzi ya serikali, hali ambayo inaelezwa kuchangia katika hatua ya kulifungia kanisa lake na kuzuiwa kwa waumini wake kuhudhuria ibada.

Kamanda Muliro ameeleza kuwa hatua ya polisi kuzingira kanisa la Gwajima na kuzuia shughuli za kidini ilichukuliwa baada ya taasisi hiyo ya kidini kufutiwa usajili na mamlaka husika.

Hata hivyo, ameongeza kuwa iwapo kanisa hilo litatumia njia sahihi za kisheria na kufanikiwa kushinda rufaa yake, basi polisi hawatakuwa na pingamizi lolote kuhusiana na kuendelea kwa ibada zao.

“Tunazingatia sheria, na yeyote anayefuata sheria hana shida nasi.

Tukipata uthibitisho wa kisheria kwamba wana haki ya kuendelea na ibada, tutaheshimu hilo,” amesema Muliro katika mahojiano na Wasafi FM.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, hatua ya serikali kuonyesha utayari wa msamaha inaweza kuwa ni ishara ya kutafuta njia ya maridhiano baina ya pande mbili zilizoingia kwenye mvutano.

Hata hivyo, wapo wanaoona kuwa suala hili lina mizizi ya kisiasa kutokana na Gwajima kujitokeza mara kwa mara kupinga baadhi ya matamko ya viongozi wa juu wa serikali.

Hali hii imezua mjadala mpana katika mitandao ya kijamii, ambapo baadhi ya Watanzania wanaunga mkono hatua ya serikali kwa msingi wa kulinda utawala wa sheria, huku wengine wakiona kuwa ni njia ya kumkomoa kiongozi huyo wa kiroho kwa misingi ya tofauti za kisiasa.

Hadi sasa, bado haijajulikana iwapo kanisa la Ufufuo na Uzima litaendelea na rufaa hiyo au kuchukua hatua nyingine za kisheria.

Wafuasi wa Gwajima wanaendelea kuiomba serikali kuangalia suala hili kwa jicho la huruma na kutambua mchango wa kiongozi huyo katika jamii ya kidini na kisiasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *