Maskini Mzize, Wingi wa Mawakala Watibua Deal Lake Zamaleki
Klabu ya Zamalek ya Misri, imesimamisha rasmi kwa muda mchakato mzima wa kunasa saini mshambuliaji nyota wa Yanga, Clement Mzize baada ya kuwepo kwa muingiliano wa kimamlaka kwa upande wa viongozi wa nyota huyo. Ambapo, hapo awali wakala mkuu wa nyota huyo alimalizana na Zamalek katika upande wa maslahi, lakini kuna wakala mpya ameingilia dili hilo na dau kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Micky Jnr, mwanahabari nguli wa habari za soka barani Afrika, Wakala mkuu wa Clement Mzize ambaye anaishi nchini Morocco, amechukua uamuzi wa kuitaka Zamalek isimamishe kwa muda dili la kumsajili nyota huyo baada ya kuwepo kwa idadi kubwa ya mawakala kudai kuwa wanamsimamia Mzize huku wakitaka kiasi kikubwa zaidi cha fedha kuliko mwanzo.
Micky ameweka wazi kuwa, kuwepo kwa idadi kubwa ya mawakala kudai wanamsimamia Mzize, kumemfanya Wakala mkuu wa nyota huyo ambaye alikuwa kiunganishi kikuu katika klabu ya Zamalek, aiamuru klabu hiyo kuacha kwa muda mchakato huo. Ikiwa ni ishara wazi kuwa amechukizwa na kitendo cha kuingiliana katika dili ambalo lilikuwa ukingoni, ambapo ni kitendo cha Mzize kusaini pekee kilibakia.
Ambapo wakala huyo, Mzize na Zamalek tayari walikuwa wamekubaliana kuwa kiasi cha dola 750,000 zitakamilisha uhamisho huo. Huku ikielezwa kuwa, katika ofa hiyo ambayo Mzize aliipokea Mei 19, 2025 majira ya 5:02 asubuhi, angepokea dola 375000 wakati wa kusaini mkataba wake. Pia, tarehe 31, Disemba 2025 angepokea tena dola 375000 kukamilisha kiasi cha dola 750,000.
Lakini, baada ya kuwepo kwa idadi kubwa ya mawakala kuingilia kati uhamisho huo, huku jina la Jasmine likiwa miongoni. Wakala huyo ameonekana kujisikia vibaya, kiasi cha kuitaka Zamalek isimamishe kwa muda uhamisho huo. Jambo ambalo imekuwa vyepesi kwa uongozi wa Zamalek kukubaliana nalo, kwani Jasmine alihitaji kulipwa pesa kubwa zaidi.