SIMBA imeumia. Mashabiki wana majonzi. Viongozi wamesalia na maswali. Lakini, katikati ya huzuni moto mpya unawashwa Msimbazi. Moto wa mageuzi na kulipiza kisasi kwa njia ya mafanikio katika michuano ya CAF msimu ujao 2025-2026.
.
Hii inatokana na Simba kupoteza nafsi ya kubeba ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika mbele ya RS Berkane ya Morocco, licha ya kutoka sare nyumbani. Simba ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0 hivyo kufanya matokeo ya mwisho kuwa kipigo cha mabao 3-1 na kuwanyima taji Wekundu hao kwa mara nyingine baada ya awali kulikosa Kombe la CAF katika fainali dhidi ya Stella Abijan ya Ivory Coast.
.
Kutokana na kukwama kuandika historia, benchi la ufundi, limewatuliza wanasimba kwa kuwaambia kuwa, wanaenda kujipanga upya na kurudi katika michuano hiyo msimu ujao wakiwa imara zaidi.
.
Simba tayari imeshakata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao ikiwa na uhakika wa kumaliza nafasi mbili za juu za Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kuikosa michuano hiyo na kuangukia Kombe la Shirikisho kutokana na kumaliza nafasi ya tatu msimu uliopita
.
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema; “Tumepambana hadi mwisho. Tulikuwa na ndoto kubwa. Lakini mpira unafundisha. Sasa tunarudi nyuma kidogo… si kwa ajili ya kukata tamaa, bali kuchaji upya. Lazima tuwe tofauti msimu ujao,” alisema Fadlu anayekuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuifikisha Simba fainali ya klabu CAF.
.
Kocha Fadlu alisisituza Tayari uongozi kwa kushirikiana na benchi la ufundi umeandaa ramani ya usajili inayoonyesha Simba haitaki tena kuwa mshiriki wa kawaida Afrika. Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya klabu, timu hiyo inatarajia kufanya usajili makini wa wachezaji kati ya watatu hadi wanne wa daraja la juu ikilenga ubora kuliko idadi. Kiungo namba 10 ni kipaumbele.
.
Ingawa Charles Jean Ahoua ameonyesha kiwango bora bado Simba inataka mchezaji mwingine mbunifu mwenye uwezo wa kusukuma mashambulizi, kutoa paši za mwisho na kuamua matokeo kwa akili na ufundi.
