
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limekanusha taarifa kuhusiana na picha mjongeo iliyochapishwa katika Mtandao wa Kijamii na mtu aitwaye Maria Sarungi akieleza kuwa Polisi amepigika Arusha.
Akitoa taarifa hiyo leo Juni 14, 2026 Kamanda wa Polisi Mkoani humo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema taarifa hiyo ni ya uongo kwani Mkoani Arusha hakuna tukio lolote lililotokea kuhusiana na Askari kupigwa.
SACP Masejo amebainisha kuwa inaonesha wazi kuwa picha mjongeo hiyo ilichukuliwa maeneo mengine nje ya nchi na kisha kutengenezewa maneno ya uongo.
Aidha, amewaomba Wananchi kupuuza taarifa hiyo, kwani mtu huyo amekuwa akiandaa na kusambaza maudhui ya uongo, uchonganishi na kutaka kuleta taharuki kwa jamii jambo ambalo ni kinyume na makuzi, mila, desturi na mifumo ya kisheria.
Jeshi la Polisi mkoani humo, limeendelea kutoa wito na onyo kwa baadhi ya watu wenye tabia kama hizo za kuandaa na kusambaza taarifa za uongo, kupandikiza chuki na kuchonganisha jamii kuacha kufanya hivyo kwani ni kinyume cha sheria.
