
Simba SC imeporomoka katika viwango vya ubora wa klabu barani Afrika vilivyotolewa na Confederation of African Football baada ya kuwa na msimu mgumu wa michuano ya kimataifa 2025/26.
Kwa mujibu wa viwango hivyo vipya vilivyotolewa baada ya kukamilika kwa nusu fainali za michuano ya CAF, Simba imeshika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 38, ikishuka kutoka nafasi ya tano iliyoshika mwaka 2025.
Katika msimu huu wa CAF Champions League, Simba ilimaliza mkiani mwa Kundi D ikiwa nyuma ya Stade Malien, Esperance de Tunis na Petro de Luanda.
Wakati Simba ikishuka, Young Africans SC imeendelea kupanda hadi nafasi ya 12 ikiwa na pointi 35, ikizipita klabu kama Wydad Casablanca, ASEC Mimosas, Orlando Pirates na TP Mazembe.
Kwa upande wa Tanzania, Azam FC imepanda hadi nafasi ya 38 sambamba na Singida Black Stars baada ya kufanya vizuri katika CAF Confederation Cup msimu huu.
Katika nafasi za juu, Mamelodi Sundowns wanaongoza viwango hivyo huku wakitinga fainali ya CAF Champions League dhidi ya AS FAR.
Kwa upande wa CAF Confederation Cup, USM Alger na Zamalek SC zimefuzu fainali.
Simba katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imefanikiwa kufika robo fainali mara tatu, huku msimu uliopita ikifika fainali ya CAF Confederation Cup chini ya kocha Fadlu Davids ambaye kwa sasa anaifundisha Raja Casablanca.
Kwa upande wa Yanga, iliwahi kufika fainali ya CAF Confederation Cup msimu wa 2022/23 chini ya kocha Nasreddine Nabi lakini kupoteza dhidi ya USM Alger.
