Tume Yafichua: Picha za AI Zilitumika Kupotosha Matukio ya Oktoba 29 – Video

Tume ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 imebaini matumizi ya teknolojia ya akili unde (AI) katika upotoshaji wa picha zilizosambaa mitandaoni, ikiwemo zile zilizodaiwa kuonyesha madhara makubwa kama maziko ya watu katika makaburi ya halaiki.

Akizungumza leo Aprili 23, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha ripoti ya Tume hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Othman Chande, amesema uchambuzi wa kina umefanyika kwa ushahidi wa kidijitali uliokusanywa.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, Tume ilikusanya jumla ya picha mnato 450 na picha mjongeo 880 kutoka vyanzo mbalimbali, zikiwemo mitandao ya kijamii, vyombo vya habari na mashuhuda wa matukio. Baadhi ya picha hizo zilikuwa zimerudiwa kusambazwa mara nyingi mtandaoni.

Amesema uchunguzi wa kisayansi uliowashirikisha wataalam waliothibitishwa umeonyesha kuwa baadhi ya picha zilikuwa halisi, lakini nyingine zilihaririwa au kutengenezwa kwa kutumia teknolojia ya AI pamoja na nusu ukweli ili kuunda simulizi potofu.

Mfano uliotajwa ni picha iliyosambaa sana ikionyesha miili ikiwa imehifadhiwa kwenye mifuko ya rangi ya bluu, ikidaiwa kuhusishwa na maziko ya halaiki. Hata hivyo, Tume imebaini picha hiyo iliwahi kutumika katika matukio tofauti duniani na si ya tukio la Oktoba 29.

Tume hiyo imeeleza kuwa hali hiyo inaonyesha jinsi teknolojia ya kisasa inavyoweza kutumika kuathiri uhalisia wa taarifa, na hivyo kuhitaji umakini mkubwa katika kuchambua taarifa zinazozagaa mitandaoni.

Related Posts