Waliomshambulia Padri Kitima Walipaswa Kuwa MahakamaniWaliomshambulia Padri Kitima Walipaswa Kuwa Mahakamani

Waliomshambulia Padri Kitima Walipaswa Kuwa Mahakamani

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Wolfgang Pisa amesema hali ya kiafya Padri Charles Kitima, katibu mkuu wa Baraza hilo, inaendelea vyema na atarejea katika majukumu yake hivi karibuni.

Padri Kitima alishambuliwa Aprili 30, 2025 na kitu butu kichwani alipokuwa kwenye ofisi za TEC Kurasini Temeke jijini Dar es Salaam na kulazwa katika Hospitali ya Aga Khan.

Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ilieleza kuwashikilia watu wawili wakishukiwa kuhusika na tukio hilo na kuwa watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.

Kufikia sasa hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na Polisi kuhusu upelelezi wa tukio lile ama kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa.

Akizungumza Jana Jumapili kwenye misa ya kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, Josephat Jackson Bududu, Rais huyo wa TEC amezungumzia afya ya Padri Kitima na matumaini yaliyopo.

Misa hiyo imeadhimishwa katika Kanisa Kuu la Mt. Theresia, Tabora ambapo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, waumini pamoja Serikali akiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi, akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kama mnavyofahamu aliumizwa, Padri anawashukuru kwa sala, yeye anaendelea vizuri, ni sala na matumaini yetu akiendelea vile atarudi kwenye majukumu yake hivi karibuni.

“Sisi tunaendela kulaani kile kitendo cha aibu, kibaya na kiovu kilicholenga kukatisha maisha ya padri wetu akiwa katika makazi na makao makuu ya baraza baraza.

“Katika utawala bora na wa sheria, wahalifu wale walipaswa wawe wameshafikishwa mahakamani mpaka sasa. Matumaini yetu uchunguzi hautachukua muda mrefu zaidi kabla ya wahusika kufikishwa mbele ya sheria,” amesema ambaye pia ni askofu wa Jimbo la Lindi.

Ameongeza kuwa ili kuwa na amani, hakuna raia atakayependa kuona wahalifu kama wale uraiani na hakuna raia ambao hawatapenda kuishi katika nchi yao katika amani, haki na ukweli.

“Wala wasingependa kuona magenge kama yale yawe hatari kwetu sisi na kwa watu wengine. Kwa wahusika pia kwa wale wanayoyazalisha, wafahamu makundi kama haya ni hatari kwao, sijui kama wanajua hivyo,” amesisitiza Askofu Pisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *