
Wanajeshi nane, wakiwemo wafanyakazi wawili wa Boeing, wamepoteza maisha baada ya ndege ya kijeshi aina ya B-52 ya Jeshi la Anga la Marekani kuanguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards, kusini mwa California.
Ajali hiyo ilitokea Jumatatu saa 11:20 kwa saa za eneo wakati ndege hiyo ikiwa katika misheni ya kawaida ya majaribio.
Kwa mujibu wa maafisa wa jeshi, ndege hiyo ilianguka na kuwaka moto mara tu baada ya kuondoka ardhini, hali iliyosababisha moshi mzito mweusi kuonekana kwa umbali mrefu.
Kanali James Hayes alisema waliopoteza maisha ni wanajeshi, wafanyakazi wa serikali na wakandarasi waliokuwa wakihudumu katika operesheni hiyo.
Hayes alieleza kuwa dalili za awali zinaonyesha ajali hiyo haikuwa na nafasi ya manusura, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo chake. Kufuatia tukio hilo, shughuli zote katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Edwards zimesitishwa kwa muda, wakati familia za marehemu zikiendelea kupewa taarifa rasmi kabla ya majina yao kutangazwa.
