Waumini wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la Askofu Josephat Gwajima lililopo Ubungo Dar es Salaam wakiwa wamekaa nje ya kanisa hilo baada ya kanisa lao kufutwa Juni 3, 2025.


Dar es Salaam. Waumini 84 kati ya 86 waliokamatwa katika Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Askofu Josephat Gwajima, wameachiwa kwa dhamana baada ya kuzuiliwa kwa muda wakituhumiwa kukiuka maagizo ya Serikali.

Waumini hao ni miongoni mwa waliokamatwa alfajiri ya kuamkia Juni 3, 2025, kufuatia mvutano uliotokea kati yao na Jeshi la Polisi, lililovamia makao makuu ya kanisa hilo yaliyopo Ubungo, jijini Dar es Salaam, na kusitisha maombi yaliyokuwa yakiendelea baada ya Serikali kulitangaza rasmi kulifuta.

Akizungumza na Mwananchi, wakili wa Askofu Josephat Gwajima, Peter Kibatala amesema jumla ya waumini 86 walikamatwa miongoni mwao 84 wameachiwa kwa dhamana jioni ya Jumatano Juni 4, 2025.

“Waumini 86 walikamatwa, wameachiwa wote kwa dhamana isipokuwa wawili ambao taarifa zao tutazitoa baadaye,” amesema wakili Kibatala.

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kuachiwa kwa waumini hao, alijibu kwa kifupi kwamba kuna tofauti kati ya kukamatwa na kushikiliwa.

Waumini hao walikamatwa kufuatia purukushani kati yao na Jeshi la Polisi, ambalo lilivamia kanisa hilo lililopo Ubungo na kusitisha maombi yaliyokuwa yakiendelea alfajiri ya kuamkia Juni 3, 2025.

Waumini hao walikuwa wakishiriki katika maombi ya kufunga kwa siku saba yaliyoanza Juni 2, 2025, lakini hayakuweza kuendelea baada ya kanisa hilo kuwekewa utepe wa zuio na kuwa chini ya ulinzi wa polisi, kufuatia tangazo la Serikali la kulifuta rasmi.

Hadi leo, Juni 5, 2025, askari wenye silaha pamoja na gari la maji ya kuwasha bado wanaendelea kuimarisha ulinzi kwenye kanisa hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *