
Wazazi wa Ashly Robinson, mshawishi wa mitindo ya maisha kutoka Marekani, wameibua maswali kufuatia kifo cha binti yao kilichotokea chini ya mazingira yasiyoeleweka wakati akiwa likizoni Zanzibar.
Katika mahojiano yao ya kwanza na CBS News, wazazi hao walisema Ashly (31) alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa pamoja na uchumba wake, lakini ghafla akafariki dunia.
Mama yake, Yolanda Endres, alisema tukio hilo limewaacha katika mshangao mkubwa, akisisitiza kuwa binti yao alipaswa kuwa katika hali ya furaha wakati huo.
Kwa mujibu wa familia, walipokea taarifa kuhusu tukio hilo kutoka kwa mchumba wake, Joe McCann, saa 11 baada ya tukio linalodaiwa kusababisha kifo hicho. Baadaye walithibitishiwa na hoteli aliyokuwa amefikia kuwa Ashly amefariki.
Jaribio la CBS News kuwasiliana na kampuni ya mchumba huyo, Asymmetric, halikufanikiwa baada ya kutopata majibu.
Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imethibitisha kifo cha raia wa Marekani huko Zanzibar, lakini haikutoa maelezo zaidi kutokana na sababu za faragha.
Tukio hilo limeibua maswali kuhusu mazingira halisi ya kifo hicho, huku familia ikiendelea kusubiri majibu ya kina kuhusu kilichompata binti yao.
Chanzo: BBC
