Moja kati ya matukio yaliyotikisa mchezo wa pili wa fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati klabu ya Simba na RS Berkane ni tukio la Fabrice Ngoma na Moussa Camara, nyota wa klabu ya Simba kupigana muda mfupi baada ya kutamatika kwa kipindi cha kwanza cha mchezo huo baada ya kutofautiana kauli.
Kupitia video fupi iliyochapishwa na Ahmed Abdallah, mtangazaji wa Wasafi FM kupitia mtandao wa Instagram Mei 24, 2025 muda mfupi baada ya matukio. Fabrice Ngoma alionekana kumuelekeza kitu Moussa Camara lakini alionekana kutokuwa tayari kukosolewa. Jambo ambalo lilifanya wawili hao waingie katika mgogoro mkubwa kiasi cha kuamuliwa.
Katika maelezo yake, Ahmed Abdallah aliweka wazi kuwa chanzo kikubwa cha ugomvi huo ni kukosekana kwa utayari wa Camara kupokea maelekezo au kurekebishwa na Ngoma kwa kile ambacho Ngoma aliamini kuwa Camara kuna sehemu aliteleza, kwahiyo hatakiwi tena kufanya makosa ya aina ile kwa usalama wao.

Lakini Camara aliona kama vile hastahili hata kidogo kurekebishwa, kitu kilichofanya wawili hao waingie kwenye mvutano mkubwa kiasi cha kuamuliwa. Tukio ambalo kwa namna moja linatajwa kuwa lingeweza kuwaondolea hali ya kupambana kwa maana tayari Berkane walikuwa na faida kubwa kupitia ushindi wao walioupata wakiwa katika ardhi ya nyumbani.
Baadhi ya wadau wa soka wameweka wazi kuwa tukio hilo halikupaswa kutokea kwa wachezaji hao. Kwa maana siyo salama kwa klabu ambayo ipo nyuma, ikiwa inatafuta nafasi ya kurudisha mabao kisha kutwaa taji lake la kwanza katika historia ya klabu tangu kuanzishwa kwake. Lakini, tayari ilikuwa imeshatokea kabla ya dakika 90 za mchezo.
Kuangalia video ya tukio bonyeza maneno ya blue hapo chini. Pia, tunaomba utuandikie maoni yako katika uwanja wa kutolea maoni.
Chanzo: Ahmed Abdallah (IG, Mei 25, 2025).