Donald Trump Amuwashia Moto Rais Ramaphosa: Kwanini Hamjamkatama Malema Kwa Kutishia Kuua Wazungu?
Rais wa Marekani, Donald Trump, amemuuliza Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa walipokutana Ikulu ya White House Marekani May 21,2025 kwamba kama Serikali yake haiungi mkono ubaguzi na mauaji ya Wazungu nchini Afrika Kusini kwanini hadi leo hawajamkamata Kiongozi wa Chama cha Economic Freedom Fighters (EFF) na Mbunge wa Bunge la Afrika Kusini Julius Malema ambaye alitangaza hadharani mbele ya umati wa Watu kuwa Wazungu wanapaswa kuuawa na kupokonywa ardhi zao.
Trump aliuliza swali hilo muda mfupi baada ya Trump kuagiza TV iwashwe na akamuonesha Ramaphosa jinsi baadhi ya Viongozi na Wanaharakati nchini mwake akiwemo Malema walivyotangaza hadharani kile Trump alichokiita ubaguzi wa Wazungu na kuwapokonya ardhi zao, ambapo licha ya kutazama video hiyo Ramaphosa aliendelea kusisitiza kwamba Serikali yake haiungi mkono mauaji ya Watu.
Trump amehoji “Kwanini hamjakamata yule Mwanaume (Malema), amesema ‘Wazungu wauawe, waueni Wazungu’ kisha anacheza huku anarudia kauli yake, sina uhakika lakini nadhani Mtu akisema waueni Watu fulani, anapaswa kukamatwa haraka, yule alikuwa anaongea kwenye uwanja wenye mamia ya Watu na kuna Wazungu wenye mashamba yao tumeona video wameuawa”
Itakumbukwa katika siku za nyuma Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alimjibu Rais Trump aliyetangaza kusitisha misaada nchini humo kisa madai ya ukiukwaji wa haki za Binadamu na Wazungu kunyanyaswa na kupokonywa ardhi wanazomiliki ambapo Ramaphosa alimtaka Trump aache kuingilia ya Afrika Kusini kwakuwa hayamuhusu na kusema ardhi ya Afrika Kusini sio ya Trump hivyo hana haki ya kuwapangia cha kufanya.
Mkutano wa Viongozi hao umeitishwa ili wazimalize tofauti zao na kurejesha ushirikiano upya, ambapo Trump alimtaka Ramaphosa kukiri kuwa Wazungu wanabaguliwa nchini mwake na alipokataa imewashwa TV na ushahidi wa nakala nyingine muhimu za karatasi na picha pamoja na video zinazoonesha mashamba ya Wazungu yanayodaiwa kupokonywa.