Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa kauli kali inayohusiana na viongozi wa CCM wanaotetea au kupitisha watu wasiofaa, na kusema wazi kuwa “hatutaki magwajima kwenye chama,” wengi waliamini kuwa alilenga moja kwa moja kwa Askofu na Mbunge wa Kawe, Josephat Gwajima.
Hili lilikuja kufuatia msimamo wa Gwajima kuhusu masuala ya haki za binadamu, ukiwemo utekaji ambao amekuwa akiukemea hadharani.
Katika majibu yake kupitia ukurasa wa Instagram, Askofu Gwajima hakusita.
Badala ya kujitetea kwa kawaida, amezindua dhana mpya inayojulikana kama Gwajimanization, ambayo anaielezea kama falsafa ya kisiasa ya kusema ukweli kwa ujasiri bila kuhofu mamlaka au matokeo yake.
Kwa mujibu wa chapisho lake, Gwajimanization ni zaidi ya kauli au kampeni – ni harakati ya kuwasha mwamko wa kisiasa miongoni mwa Watanzania kwa lengo la kusimamia haki, uwazi, na maslahi ya taifa dhidi ya dhuluma au matumizi mabaya ya madaraka.
Gwajima alionekana akiwa na kipaza sauti, akizungumza kwa msisimko mkubwa, huku akihimiza kila Mtanzania mwenye dhamira safi kuwa na ujasiri wa kusema ukweli, hata kama ukweli huo unaweza kumkera aliye madarakani.
Anafafanua kuwa falsafa hiyo inalenga kuamsha ujasiri wa kupambana na mifumo ya udhalimu, na kuweka mbele maslahi ya wananchi kabla ya maslahi binafsi.
Chapisho hilo limeibua mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii.
Wapo wanaomuunga mkono wakimpongeza kwa ujasiri na msimamo thabiti, wakisema sauti yake inawakilisha wananchi wasio na mahali pa kusemea.
Hata hivyo, wapo pia waliomkosoa, wakisema kuwa mbinu zake zinaweza kuhatarisha mshikamano ndani ya chama au kuonekana kama upinzani wa ndani.

Licha ya maoni hayo tofauti, ni wazi kuwa Gwajima ameweka wazi msimamo wake, na anazidi kujionyesha kama mwanasiasa asiyetetereka, anayejitokeza kuwa sauti ya kukosoa kwa uwazi bila woga.
Hii inaonesha kuwa mvutano wa kisiasa ndani ya chama unaweza kuchukua sura mpya, hasa ikizingatiwa kuwa matamshi haya yanatoka kwa viongozi wakuu wa taifa.
Je, hatua ya Gwajima itaungwa mkono na wengi au italeta mgawanyiko zaidi? Muda ndio utakaotoa majibu.
Putting Garlic in Hot Water? Old Trick Returns in Local Villages
bio-nutrabalance.
by TaboolaSponsored Links