Haji Manara, msemaji wa zamani wa klabu ya Simba SC, ameibuka na kuwatia moyo mashabiki wa timu hiyo kuelekea mchezo muhimu wa marudiano dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco, utakaochezwa Jumapili tarehe 25 Mei visiwani Zanzibar.

Kupitia ujumbe wake wenye lugha ya kuchangamsha, Manara aliwahakikishia mashabiki kuwa wasiwe na hofu kuhusu vitisho vya Waarabu, akiwataka waamini kuwa Simba ina uwezo wa kushinda. “Hiyo ni Mikwala tu ya Waarabu wanapotaka jambo lao flani… Wanakuwa na Mikiliti ya kila aina, isiwatishe,” aliandika Manara kwa ucheshi.

Akitambua ugumu wa mchezo huo, Manara alibainisha kuwa kuna mchezaji wa RS Berkane mwenye uwezo mkubwa, hasa katika safu ya ulinzi, lakini akasisitiza kuwa Simba inaweza kumdhibiti. “Ila kuna Njemba imesimama kwa pembeni, ina Utege flani hivi wa kifull beki, kama mnaweza mzuieni asitue Zanzibar, mtanishukuru baadaye,” aliandika kwa kejeli.

Manara pia alidokeza kuwa mashabiki wanapaswa kumuangalia kwa makini mchezaji mmoja wa RS Berkane ambaye alimtaja kwa utani kuwa “Anko Tege Yeye”, akidai kuwa ndiye hubeba mikoba ya timu hiyo.

Mchezo huu ni wa muhimu kwa Simba SC, kwani matokeo yake yataamua ni timu ipi itaendelea kwenye mashindano ya kimataifa. Mashabiki wamehamasishwa kujitokeza kwa wingi na kuisapoti timu yao kwenye dimba la Amaan, Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *