Alice Iyabo Ojeli, maarufu kama Iyabo Ojo, ni jina kubwa kwenye tasnia ya filamu Nigeria (Nollywood). Akiwa na uzoefu wa zaidi ya miaka 25, ameigiza zaidi ya filamu 150 na kutayarisha zaidi ya filamu 14, hatua iliyomfanya kuwa miongoni mwa wanawake wenye ushawishi mkubwa Afrika.
Alizaliwa Desemba 21, 1977 (miaka 48), Lagos, Nigeria, na ni mtoto wa mwisho kati ya watatu. Akiwa na asili ya Abeokuta (Jimbo la Ogun), Iyabo alisoma National College, Gbagada na baadaye akapata HND ya Estate Management kutoka Lagos State Polytechnic. Mapenzi yake ya sanaa yalianza shuleni kupitia vikundi vya tamthilia na mwaka 1998 akaanza rasmi sanaa kupitia Actors Guild of Nigeria.
Mwaka 2004 alianza kutengeneza filamu zake mwenyewe kama Bolutife, Esan na Okunkun Biribiri, ambazo zinahamasisha mabadiliko ya kijamii. Filamu Silence (2015) na Labake Olododo (2025) zimekuwa na mafanikio makubwa.
Tanzania, Iyabo anafahamika pia kama “mama mkwe wa Jux”, msanii wa Bongo Fleva, jambo lililoleta umaarufu wake zaidi Afrika Mashariki ni #JP2025. Mbali na burudani, Iyabo anasifika kwa kusimamia haki za watoto, kupinga ukatili wa kijinsia, na kuikosoa serikali kuhusu kodi ya mamilioni ya Naira.
Mwaka 2011 alianzisha taasisi ya Pinkies Foundation kusaidia watoto wenye mahitaji maalum na familia zisizojiweza. Kupitia taasisi hii, amegusa maisha ya wengi.
Ameshinda tuzo kadhaa ikiwemo Best Supporting Actress (2012) na anaendelea kuwa nembo ya mabadiliko kwenye filamu na jamii. Iyabo Ojo ni mfano wa mwanamke mwenye uthubutu, mwenye vipaji vingi na moyo wa kusaidia wengine.