UKIONDOA jina la kiungo Stephanie Aziz KI aliyeuzwa Morocco, staa atakayefuata sasa ni straika Clement Mzize aliyebakiza wiki moja tu kuuzwa moja ya nchi ya Afrika Kaskazini baada ofa tatu kutua klabuni hapo kwa Waarabu kuongeza dau ili kumng’oa Yanga.
Mzize anayemiliki mabao 13 na asisti tatu katika Ligi Kuu kwa sasa amekuwa kwenye rada za klabu kadhaa, lakini inaelezwa kwa sasa mipango iliyopo ni kwamba muda wowote ataondoka Yanga kwa kuuzwa na klabu hiyo kama ilivyokuwa kwa Aziz KI.
Ingawa mabosi wa Yanga wanafanya siri juu ya biashara hizo, lakini Mzize anahesabu siku tu kuuzwa baada ya klabu tatu za Wydad Athletic iliiyomnunua Aziz KI, Zamalek ya Misri na Al Hilal Tripoli ya Libya zote zikifikia dau ambalo Yanga inalitaka.
Taarifa kutoka kwa wasimamizi wa mshambuliaji wa huyo ni kwamba klabu hizo tatu kila moja imekubali kutoa Dola 500,0000 (takriban Sh1.4 bilioni) kuwania saini ya Mzize na uongozi wa Yanga umeshawishika juu ya ofa hizo.