Kijana Aliyelelewa na Nyani Porini Yuko Dar Akipambania Maisha
KATIKA mitaa ya Segerea jijini Dar es Salaam, kijana Baraka Rose, anaishi na ndiko anakofanya harakati za kujitafutia kipato, akijiajiri mwenyewe kushona viatu
Baadhi ya wakazi wa eneo hilo kila walipoona walipita na kusalimia kwa kuwa baadhi yao wanamfahamu kwa vile ni muumini mwenzao katika kanisa lilipo Chang’ombe Tabata kwa kipindi kirefu.
Katika mahojiano kuhusiana na maisha yake, hasiti kuweka wazi kuwa ni mwenyeji wa mkoa wa Kigoma na ni mtoto aliyelelewa na nyani porini kwa miaka mingi iliyopita wilayani Bukombe huko Shinyanga.
Kwa ujumla licha ya kuwapo maelezo kuhusu safari yake ya kukulia mikononi mwa nyani, anasema aliokotwa na nyani huyo baada ya kutupwa akiwa bado mchanga.
Lakini ukweli haijulikani, alitupwa baada ya kuzaliwa, aliibwa na nyani kijijini au walimshambulia mlezi au mama yake wakakimbia na mtoto.
Baraka anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 35 anasema hamfahamu mama yake wala ndugu zake na kwamba anajishughulisha na kushona viatu kwa ajili ya kupata fedha za kununua chakula.
Anasema pia anatengeneza mabanda ya kufugia kuku, mabata, sungura na ufundi wa kupaua nyumba na kuweka dari majumbani.
Baraka, anasema ujuzi wa kazi hizo ameupata kutokana na kujichanganya mitaani kwa kuwangalia mafundi wengine kile wanachofanya kwenye kushona viatu, kuezeka, kutengeneza dari na kupaka rangi.
Anasema anatangaza kazi yake ya kushona viatu kwa kutumia kipaza sauti na fedha anazopata ananunua chakula na mahitaji mengine madogo.
Anaeleza kuwa usiku analinda maduka yaliyopo maeneo ya Kimanga Tabata na analazimika kufanya hivyo kwa sababu hana sehemu maalumu ya kuishi kutokana na kukosa kipato cha kulipa kodi ya nyumba.
“Hela niyopata ni kidogo sana kwani inatosha kwa ajili ya kununua chakula pekee na si vinginevyo,” anasema Baraka.
Kijana Baraka anaendelea kusema kuwa anapenda kuishi maisha ya kifahari kama ilivyo kwa vijana wenye umri kama wake na anampenda Mungu akimuomba amjalie kuwa na mke mwema ambaye ataishi naye katika maisha yake yote.
Vilevile anasema anatamani kumiliki nyumba ya kisasa na gari kama ilivyo kwa baadhi ya wananchi.
“Tatizo langu ni kuwa uwezo wa fedha ambazo zingeniwezesha kufanya mambo hayo yote sina kwa sababu ya kukosa elimu, ningepata niwe msomi kama ilivyo kwa wengine,” anasema Baraka.
“Napenda sana kusoma nikiwaona watoto wanavyoenda shule na vijana wengine vyuoni wakisoma, lakini ndiyo hivyo. Nawaomba wasamaria wema wajitokeze kunisaidia kujiunga na mafunzo ya ufundi kwa kuwa ni kazi ninayoiweza lakini sina vyeti,” anaongeza kusema.
AKUMBUKA ALIKOTOKA
Akisimulia jinsi alivyochukuliwa kutoka mikononi mwa nyani na kulelewa na binadamu, Baraka anasema polisi walimwambia kuwa waliamua kumpiga risasi nyani, ambayo ilimjeruhi kwenye kidole cha mguu wa kushoto ndipo alipoanza kulelewa na binadamu.
Anasema nyani huyo, alipigwa risasi na askari wa wanyamapori wa wilaya ya Ushirombo, wakati huo anaambiwa alikuwa anamnyonyesha. Hata hivyo, anasema aliambiwa kuwa askari hao walipata shida kumpata kutokana na nyani aliyekuwa akimlea mwituni hadi alipofikisha miaka mitano kukimbia kila alipokuwa anawaona walinzi hao wa wanyama pori.
Anaendelea kusema kuwa baada ya purukushani hizo, askari hao walimchukua na kumpeleka Hospitali ya Wilaya ya Bukombe ambako alilelewa na kupatiwa matibabu na huduma nyingine za kiafya na kijamii.
Anadai kuwa aliondoka kwa mlezi aliyekuwa anamtunza kwa sababu ya kumtusi kuwa ni nyani kasoro mkia hivyo, akaamua kuondoka akimiani kuwa hathaminiwi na historia yake imetumiwa kumnyanyasa.
MABADILIKO Pamoja na Baraka kuishi mitaani na binadamu, bado anatumia ishara alizozoea wakati akiishi na nyani porini ambazo ni pamoja na namna walivyokuwa wakizungumza, kupeana ishara kwa kupiga mluzi kama ishara ya kwenda kula, kutafuta chakula, kuparamia miti na kucheza.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kimanga, Pastory Kyombya, anakaririwa akisema Baraka alikuwa akilelewa na mkazi mmoja wa eneo hilo, baada ya kukabidhiwa jukumu hilo na uongozi wa wilaya ya Bukombe.
Anasema wakati ule aliyekuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukombe Richard Nhende, alimpa jukumu hilo mkazi baada ya kukamilisha taratibu za kisheria.
Aidha, anasema mwananchi huyo alimchukua na kumlea baada ya kuambiwa na mwenzake kuhusu taarifa zake baada ya kumpoka nyani