Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba SC, Mohammed Dewji, ameandika barua ya wazi akionesha masikitiko yake makubwa kuhusu uamuzi wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) wa kupeleka mchezo wa marudiano wa fainali ya Kombe la Shirikisho visiwani Zanzibar badala ya kuchezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Dewji amesema maamuzi hayo hayakuwatendea haki Simba na yamewaumiza mashabiki na Watanzania kwa ujumla.
Katika barua hiyo, Mo Dewji ameeleza kuwa klabu ya Simba ilifanya juhudi kubwa kuhakikisha mechi hiyo muhimu inachezwa katika uwanja wao wa nyumbani kwa lengo la kutoa nafasi kwa mashabiki wengi kushuhudia tukio hilo la kihistoria. Hata hivyo, licha ya jitihada hizo, CAF imeendelea kusisitiza msimamo wao wa kuandaa mechi hiyo Zanzibar.
Amesema kuwa kuna mazingira yasiyoeleweka yaliyopelekea uamuzi huo, ikiwa ni pamoja na taarifa muhimu za CAF kuvuja mitandaoni kabla ya kutolewa rasmi. Hali hiyo imeibua maswali mengi kuhusu uwazi wa mchakato wa maamuzi ndani ya CAF.
“Bila shaka matokeo haya ni ya kusikitisha, si kwa Simba tu bali hata kwa mashabiki wetu na kwa wale wanaojitoa kwa juhudi kubwa kuandaa tukio hili katika historia ya Simba na Tanzania. Kwa mtazamo wangu wa binafsi, hatukutendewa haki,” alisema Dewji.
Hata hivyo, Dewji amesisitiza kuwa Simba haijawahi kutegemea mazingira ya faraja kupata ushindi, bali imekuwa ikiongozwa kwa imani, uzalendo, na nguvu ya watu wake. Amesema kuwa timu hiyo itaelekea Zanzibar kwa wajibu na dhamira ya kuiwakilisha nchi kwa fahari kubwa, bila kuyumbishwa na changamoto zilizopo.
“Zanzibar tunaenda kwa wajibu, si kwa hiari. Tutaenda na moyo wa kujituma na kuhakikisha tunaitangaza vyema Simba na Tanzania katika ngazi ya kimataifa,” aliongeza.
Kauli ya Mo Dewji imeibua hisia kali miongoni mwa mashabiki, huku wengi wakieleza kuwa Simba imeonesha ukomavu kwa kukubali hali hiyo lakini bado wanatarajia kuona haki ikitendeka siku za usoni

