Katika kile kinachoonekana kuwa mvutano wa kisiasa unaochukua sura ya wazi, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, amemshambulia vikali mkuu wake wa mkoa wa Arusha wa sasa Paul Makonda kwa kauli alizozitoa kuhusu maendeleo ya Arusha.
Akizungumza na vyombo vya habari mkoani Arusha, Gambo alisema kuwa Makonda anapaswa kuangalia masuala ya msingi badala ya kujihusisha na siasa zisizo na tija kwa maendeleo ya wananchi.
Katika mahojiano hayo yaliyovuta hisia za wengi, Gambo alieleza kuwa Makonda “anatafuta aibu ukubwani” kwa kutaka kuleta migogoro na hali ya taharuki isiyo ya lazima katika eneo ambalo limekuwa na maendeleo ya kutosha bila mchango wake wa moja kwa moja.
“Hii siyo sehemu ya kuja kutafuta umaarufu kwa kuleta maneno yasiyo na msingi,” alisema Gambo kwa msisitizo huku akiwa amezingirwa na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali.
Kauli hiyo ya Gambo imeibuka baada ya Makonda kutoa matamshi yanayodaiwa kubeza juhudi za maendeleo zilizofanyika mkoani Arusha, jambo ambalo limeibua maswali kuhusu nia ya kauli hizo.
Gambo alisema kuwa Arusha imekuwa miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa kasi ya maendeleo na haitakubali kuyumbishwa na siasa za matusi, chuki na upotoshaji.
“Ukiangalia hali halisi ya maendeleo ya Arusha, hakuna nafasi ya watu wanaotafuta sifa kwa kutumia njia za kubeza wengine. Tunahitaji siasa safi, siyo siasa za kugombanisha watu,” aliongeza Gambo.
Aidha, Gambo alitumia nafasi hiyo kuwasihi viongozi wa kisiasa kujikita kwenye ajenda za kuunganisha Watanzania badala ya kuwagawa kwa kutumia majukwaa ya siasa.
“Nawaomba wanasiasa, tuache mambo ya majibizano yasiyo na tija. Watanzania wanahitaji huduma bora, siyo malumbano yasiyoisha,” alisema.
Hali hii imeendelea kuzua mijadala mitandaoni na kwenye majukwaa ya kisiasa, ambapo baadhi ya wananchi wameeleza kuunga mkono msimamo wa Gambo, huku wengine wakitaka viongozi hao wawili kuweka tofauti zao pembeni na kushirikiana kwa ajili ya maslahi ya taifa.
Mvutano huu unaashiria changamoto kubwa zinazoukumba ulingo wa siasa za ndani ya vyama nchini, ambapo mara nyingi masuala binafsi huzidi uzito wa masuala ya maendeleo ya wananchi.
Wakati siasa za majibizano zikiendelea, macho na masikio ya wengi sasa yanamwangalia Makonda kama atajibu kwa hoja au ataendelea na msimamo wake.
Tukutane kwenye comments section tupe maoni yako kulingana na kinachoendelea kuhusiana na sakata baina ya wawili hawa Makonda Vs Mrisho Gambo.