Simba Kikaangoni, CAF Waanza Kuichunguza Vurugu Mechi ya Fainali Shirikisho
Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) limeanza uchunguzi kuhusu matukio yaliyotokea Zanzibar jana katika mchezo uliowahusisha timu ya RS Berkane na Simba SC. Kwa mujibu wa taarifa, RS Berkane waliwasilisha malalamiko yao CAF wakidai walizuiliwa kwa zaidi ya saa nne katika uwanja wa ndege bila kupokewa na wenyeji .
Aidha, CAF haikuridhishwa na tabia ya timu ya Simba wakati wa mchezo, ambapo walielezwa kuwa na vitendo vya utovu wa nidhamu kutoka kwa wachezaji na benchi la ufundi. Pia, baadhi ya mashabiki walisikika wakimzomea na kumkejeli Rais wa CAF na msafara wake .
Vilevile, uchunguzi mwingine utafanyika kuhusu kile kilichotokea katika vyumba vya kubadilishia nguo, ambapo watu wasiojulikana waliingia katika chumba cha waamuzi, jambo ambalo linakiuka kanuni za mchezo .
Kamishna wa mechi pamoja na mwamuzi tayari wamewasilisha ripoti zao kwa CAF mapema asubuhi. Inatarajiwa kuwa CAF itachukua hatua na kutoa adhabu kwa watakaobainika kuhusika na vurugu hizo.