Tusikubali Dabi ya Simba na Yanga Ishushwe Thamani

MATOKEO Yanga Vs Simba Leo Tarehe 16 September 2025

Mchezo wa Kariakoo Dabi unaendelea kubeba hadhi ya juu zaidi ndani ya Ligi Kuu Bara na ligi nyingine, ukizikutanisha timu pinzani wa jadi, Simba SC na Yanga SC. Ni mchezo ambao si tu unakuwa na pointi tatu, bali pia hubeba heshima, historia na fahari ya mashabiki wa pande zote mbili.

Msimu huu tayari tumeshuhudia michezo miwili kati ya miamba hiyo. Dabi ya kwanza ilichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ikiwa ni Ngao ya Jamii, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0. Baadaye, timu hizo zilikutana tena katika duru la kwanza la Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, mechi iliyomalizika kwa matokeo ya 0-0.

Kama Simba jana ilitinga fainali ya michuano ya Muungano basi tutashuhudia Dabi nyingine Aprili 29, 2026 na hivyo tutakuwa na uhakika wa kuziona mechi nne za Dabi msimu huu.

Pia Mei 3, 2026, Simba ni wenyeji wa mchezo wa ligi na wameamua kuipeleka dabi hiyo kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam ikiwa ni mara ya kwanza mchezo mkubwa wenye hadi hiyo ukipigwa kwenye uwanja huo. Uamuzi huo umetokana na sababu kwamba Uwanja wa Benjamin Mkapa unaendelea kufanyiwa marekebisho ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya michuano ya AFCON 2027 ambayo itafanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda.

Hata hivyo, uamuzi huo umeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka. Wapo wanaodai kuwa kuhamisha dabi hiyo kutoka uwanja wenye uwezo wa kubeba zaidi ya mashabiki 60,000 hadi ule wa watu 10,000 ni kama kuishusha hadhi ya mchezo huo mkubwa ambao umekuwa ukifuatiliwa na mashabiki wengi. Hoja yao inajikita katika ukweli kwamba Kariakoo Derby ni tukio la kitaifa linalovutia mashabiki kutoka pembe mbalimbali za Tanzania na nje ya hapo kwani kuna wengine wamekuwa wakitoka Kenya, Uganda na hata nje ya hapo kwa ajili ya kutazama mchezo huu.

Ni kweli kwamba hata Yanga walifanya uamuzi kama huo walipopeleka dabi Zanzibar, ambapo New Amaan Complex una uwezo wa kuchukua takribani mashabiki 14,000. Hivyo, Simba wanaonekana kufuata mkondo huo kwa kupunguza zaidi idadi ya watazamaji hadi 10,000. Lakini swali la msingi linabaki, kama huu ni muelekeo sahihi wa Dabi ambayo imekuwa maarufu kwa miaka mingi.

Uhalisia ni kwamba maamuzi haya yanawanyima maelfu ya mashabiki nafasi ya kushuhudia moja kwa moja pambano hilo, lakini pia wengi ambao watapata nafasi ya kwenda kwenye mchezo huo siyo wale watu wa soka haswa kwa kuwa itailazimisha timu mwenyeji kuweka viingilio vikubwa ili kuepuka kundi kubwa la mashabiki. Kupunguza uwezo wa uwanja kunawanyima fursa hiyo na kupunguza pia mapato ya klabu na wadau wengine wa soka.

Hali hii inapaswa kuwa somo kwa mamlaka husika na wadau wa michezo nchini. Tanzania inahitaji kuwa na viwanja vingi vyenye ubora na uwezo mkubwa wa kuchukua mashabiki ili mechi kubwa kama hizi ziweze kufanyika bila changamoto. Soka limekuwa sekta inayokua kwa kasi, na mahitaji ya miundombinu bora hayaepukiki.

Kwa mtazamo mpana, Kariakoo Derby haipaswi kuonekana kama mechi ya kawaida inayoweza kuchezwa popote, ni vizuri pia Shirikisho la Soka Tanzania TFF pamoja na Bodi ya Ligi wakaja na kanuni maalumu kuhusu mchezo huu ambayo itaeleza ni uwanja wa namna gani unafaa kwa mchezo huu badala la kuachiwa mwenyeji achague kwa kuwa kuna siku utapelekwa hata kwenye uwanja wa mashabiki 4,000.

Lakini pia kujenga viwanja vingi vinavyoweza kubeba mashabiki wa kutosha ni jambo la msingi sana, kwa kuwa kuna wakati hata Uwanja wa Mkapa pamoja na kuchukua mashabiki 60,000 ulikuwa ukijaa na mashabiki kuelezwa kuwa tiketi zimeshamalizika.

Ni wakati sasa kwa wadau, Serikali kuchukua hatua na kuanza kufikiri kuwa tunatakiwa kuwa na viwanja vya namna gani kwa aina ya mashabiki tulionao. Kama tunataka kuiendeleza hadhi ya dabi hii na soka la Tanzania kwa ujumla, basi uwekezaji katika viwanja bora na vikubwa ni jambo lisiloweza kuepukika

Related Posts