John Mrema: Madeni Chanzo cha Youtube ya Chadema na Mitandao ya Kijamii Kutokufanya Kazi
Akisisitiza kuwa madai ya Kuporwa kwa Kurasa za mitandao ya kijamii na Akaunti ya Youtube ya Chadema havimuhusu, Aliyekuwa Mkurugenzi wa Itifaki, mawasiliano na mambo ya nje Chadema Bw. John Mrema, amewataka wanachama wa Chama hicho kumuuliza Makamu Mwenyekiti wa bara John Heche pamoja na katibu Mkuu wao Bw. John Mnyika kuhusu hatma ya kurasa hizo kwani wanaufahamu ukweli wote.
Mrema kupitia Chapisho lake kwenye mtandao wa X, amemtaka pia Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania bara Bw. John Heche kutoa ushahidi hadharani wa yeye kuhusika na uendeshaji wa akaunti za Chama na ikiwa yeye ndiye aliyeficha nywila za akaunti za Chama hicho kama ambavyo amekuwa akidai kwenye mazungumzo yake.
“Kwamba nilikuwa pia napokea milioni tatu kila mwezi ni uongo na udhalilishaji kwani sijawahi kulipwa chochote kutokana na akaunti hizo. Hivyo basi namtaka John Heche aweke ushahidi hadharani juu ya madai haya ya uongo dhidi yangu.” Amesema Mrema.
Mrema amesisitiza kuwa anaendelea kushauriana na wanasheria wake, juu ya hatua nzuri za kuchukua ili kukomesha uongo huo ambao unasambazwa kwa lengo la kile alichokiita kumchafya mbele ya umma.
Akizungumzia Akaunti hizo, Mrema ameeleza kuwa akaunti ya Youtube inaendeshwa na Afisa wa Chama Abdulkareem Muro, na ambaye ndiye mfunguzi wa akaunti hiyo na mara zote amekuwa akiiendesha.
“Heche aliongea na AbdulKareem na akaelezwa kuhusu madai ambayo Abdul anayadai Chadema, akitaka alipwe ili awape Password. Ni muhimu Heche akaeleza umma wamefikia wapi kwenye mazungumzo yao na sio kunisingizia.” Ameandika Mrema.
Kuhusu Akaunti ya Instagram, X na Facebook, Mrema amebainisha kuwa akaunti huzo zilikuwa zinaendeshwa na Afisa aitwaye Appolo Boniface na ndiye mwenye nywila za akaunti hizo, akisema akaunti ya X ilifungwa na Kampuni inayomiliki Mtandao huo, suala ambalo Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika analifahamu na anapaswa kulizungumzia kwa umma badala ya kuacha uzushi uendelee kutamalaki kwenye mitandao, ikimtuhumu yeye kuikwapua akaunti hiyo ya X.