Msanii maarufu wa singeli Nchini, Msaga Sumu ameripotiwa kupata ajali jana Mei 16,2025 wakati akirejea Dar es salaam akitokea Wilayani Namtumbo kutumbuiza kwenye mkesha wa mwenge na kuumia sehemu mbalimbali za mwili na kupelekwa katika hospitali ya ya Wilaya ya Tunduru na kupata matibabu ya awali kabla ya kufikishwa Hospitali ya MOl, Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, Ngollo Malenya amesema “Msaga sumu alikuja Wilaya ya Namtumbo Mei 15, 2025 kwa ajili ya kutumbuiza usiku wa mwenge wa uhuru ambao ulifika Namtumbo na baadaye Mei 16, 2025 asubuhi baada ya kumaliza shughuli yake alianza safari kuelekea Dar es salaam kupitia barabara ya Tunduru”
“Walipofika Kijiji cha Azimio, Kata ya Mtina Wilayani Tunduru ndipo ajali ilipotokea na Msagasumu aliumia na kukimbizwa haraka Hospitali ya Wilaya ya Tunduru na kupata matibabu ya awali ambapo kwenye paji la uso alichanika na akashonwa hapohapo Tunduru Hospital”— amesema DC Ngollo
“Pia ana maumivu kwenye mbavu hivyo akasafirishwa na gari la ugonjwa kuelekea Dar es salaam kwa matibabu zaidi, na mpaka sasa hivi ameshafika Hospitali ya MOl kwa ajili ya uchunguzi wa ziada lakini so far nimepata taarifa anaendelea vizuri na pia matibabu ya awali yamemsaidia” — amesema DC Ngollo