Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (Tanganyika Law Society – TLS), Boniface Mwabukusi amejitokeza kulizungumzia sakata la kusitishwa kwa usajili wa kanisa la Askofu Josephat Gwajima, akisema hakuna sheria iliyovunjwa na kiongozi huyo wa kidini kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni kuhusu utekaji na kupotea kwa watu.
Kupitia ukurasa wake wa X, Mwabukusu amesema kuwa Msajili wa Jumuiya na Taasisi za Kidini anao uwezo wa kisheria wa kusitisha au kufuta usajili wa taasisi yoyote iwapo itakiuka katiba na kanuni zake au kuacha kutekeleza malengo ya msingi ya kusajiliwa kwake.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa kabla ya hatua kama hiyo kuchukuliwa, kuna taratibu za kisheria na kikanuni ambazo lazima zifuatwe kwa umakini.
“Kukemea utekaji au kutowajibika kwa viongozi wa kisiasa ni wajibu wa msingi wa kibiblia, kikanisa na kikatiba,” amesema Mwabukusu, akisisitiza kuwa kauli za Askofu Gwajima hazikiuki sheria, bali ni maoni, ushauri na wito wa kulinda jamii dhidi ya vitendo viovu.
Katika ujumbe huo, Mwabukusu pia amekosoa kile alichokiita tabia ya kusambaza barua zisizo rasmi na zenye upotoshaji kuhusu suala hilo, akisema Watanzania wanapaswa kuachana na ushabiki wa matukio yasiyo na maana badala yake wajikite katika masuala ya msingi.
“Tumekuwa na ujinga wa kupenda matukio na vitu vya hovyo hovyo kuvipa muda. Mambo ya msingi wala hatuhangaiki nayo,” amesema kwa ukali.
Ameongeza kuwa badala ya kuendekeza propaganda, jamii inapaswa kupaza sauti kudai uwajibikaji kuhusu watu waliotekwa au kupotea.
Kauli hii ya Mwabukusu inakuja wakati mjadala kuhusu uhuru wa maoni kwa viongozi wa kidini ukizidi kushika kasi, huku baadhi ya wananchi wakitaka haki ya kutoa maoni iheshimiwe bila hofu ya hatua za kisiasa.