Siyo Sawa Ibraah Kuondoka Bure Label ya Konde Gang, Lebal Sio THT
Kuna watu wataona kama nina roho mbaya lakini ukweli lazima usemwe, suala la Harmonize kushauriwa amuache Ibraah aondoke bila kulipa hela yoyote Konde Gang wala siyo sawa, mikataba ilikuwa wazi kabisa na inaeleweka, Ibraah alisaini kwamba ikitokea anataka kuondoka kabla ya mkataba kuisha basi atalipa kiasi fulani, sasa inashangaza kuona ameondoka bure bila kulipa chochote.
Unajua ndiyo maana Muziki wa Bongo kuendelea ni vigumu kwa sababu tunaweka ushikaji mbele na tunaendekeza busara itumike kuliko Sheria kwenye kesi kama hizi. Binafsi naamini Harmonize amepoteza muda na pesa yake kubwa ili kujenga brand ya Ibraah, kuna uwezekano mkubwa Harmonize hajarudisha hata robo ya alichowekeza kwa Ibraah sasa amekubali vipi kumuachia Ibraah bure hivi?
Tunavunja moyo Matajiri wanaotaka kuwekeza kwenye muziki maana na wao wanapata picha halisi yakitokea mambo kama haya watashauriwa busara itumike na Wasanii waliowajenga kwa jasho na pesa zao wataondoka bure kama Ibraah.
Tatizo hizi Lebo tunazichukulia kama kituo cha msaada, jamani Lebo siyo THT au Mkubwa na Wanawe, tofautisheni kati ya lebo na vituo vya kuelea vipaji, lebo ni biashara ambayo mikataba ndiyo inaamua kila kitu, hapa hakuna mambo ya busara kutumika, kwanini busara hizi hazikutumika kwa Harmonize na Rayvanny wakati wanaondoka WCB? maana wao wametoa Mamilioni ya kutosha ili kuvunja mikataba yao.
Baada ya sakata hili, Harmonize usikate tamaa, endelea kuinua vijana wengine kwani Binadamu wanaweza wasikupongeze lakini tambua kuwa mbali na Diamond Platnumz, wewe pia una mchango mkubwa sana kwenye tasnia, Ibraah na Anjella hakuna aliyewajua ila kupitia wewe hivi sasa Tanzania nzima wanajulikana, wanapata mpaka uwezo wa kujiamini kuwa wamekua na wanataka waondoke.
By Hopetygaz